Golden Tears

Kila kitu kinabadilika maishani mwake. Baada ya kutembea na wanaume wengi huku akiwa na ndoto ya kupata mtoto, muigizaji wa kike mwenye jina kubwa, Goodness anashindwa kutimiza ndoto hiyo kwani kila mwanaume anayekuwa naye, anamuacha bila kumuachia mtoto.Baada ya kutembea na mwanamuziki aliyekuwa akitikisa, Golden na kuoana naye, hatimaye Goodness anafanikiwa kupata watoto, ila tatizo ni pale anapoambiwa kwamba watoto hao wameungana.
Japokuwa anahuzunika anakubaliana na ukweli kuhusu watoto hao.Mume wake, Golden anataka kuwaua watoto hao lakini bahati mbaya anajichoma sindano yenye sumu na kufariki.Oparesheni ya kutaka kuwatengenisha watoto hao inafanyika lakini inashindikana na hivyo kusafirishwa kupelekwa nchini India.
Huko nako oparesheni inashindikana hivyo anawarudisha watoto wake nchini Tanzania. Safari imeanza, mamilioni ya watu wamejipanga kutaka kumpokea Goodness ambaye yupo na rafiki yake wa siku nyingi, Kei.
Goodness amefika nchini Tanzania, watu wanampungia mikono ya kumkaribisha, anapofika nyumbani, anaamua kuwaoneshea watoto hao jamaa na marafiki wa karibu, kila mmoja anapowaona anasisimka, wakaamini kwamba kweli watoto walikuwa wameungana na hazikuwa taarifa za kubuni magazetini.
SONGA NAYO....
Ilikuwa ni picha iliyomsisimua kila mmoja, kila walipokuwa wakiwaangalia watoto wale, waliihisi miili yao ikiwasisimka kupita kawaida. Ni kweli walikuwa watoto wazuri ambao muda wote walionekana kutabasamu lakini kuungana kule kulimsikitisha kila mmoja.
Ingawa watoto wake walikuwa katika hali ile, Goodness alikuwa akitabasamu tu, alikuwa ameshaizoea hali waliyokuwa nayo watoto wake hivyo hata alipowaona kwa mara nyingine mahali pale, kwake ilionekana kuwa kawaida sana.
Hakukuwa na mwandishi wa habari ndani ya nyumba hiyo na hata watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo hawakutakiwa kupiga picha yoyote ile kwani Goodness hakuwa tayari kuwaanika watoto wake katika chombo chochote cha habari.
“Ni watoto wazuri mno,” alisema Aminatha, machozi yalikuwa yakimlenga, kila alipokuwa akiwaangalia watoto wale, alikuwa akijisikia uchungu moyoni. “Wamefanana na mama yao na kwa mbali wamechukua sura ya baba yao,” alisema PJ, mmoja wa waigizaji waliokuwa wakivuma sana nchini.
Siku hiyo ilifanyika sherehe ndogo ya kumkaribisha Goodness nchini Tanzania mara baada ya kuishi nchini India kwa takribani miezi kumi. Watu walikula na kunywa huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha.
Kwa Goodness, muda wote bado tabasamu lake lilionekana usoni mwake, alifurahi kurudi nchini Tanzania kuendelea na maisha yake ya uigizaji.
Siku iliyofuata, magazeti yakawa yametoa taarifa kuhusu ujio wa Goodness nchini Tanzania. Picha za watu waliokuwa wamejipanga barabarani zilikuwa zikionekana katika kila gazeti.
Kwa wale wa mikoani ambao hawakuwa wakifahamu kuhusiana na umati wa watu hao, wakabaki wakishangaa, hali ile ilimshangaza kila mmoja, hapo ndipo ikajulikana ni kwa jinsi gani Goodness alikuwa akipendwa.
Watu walitaka kufahamu mengi kuhusu ujio wa Goodness nchini Tanzania. Magazeti yote yaliyokuwa na habari kuhusiana na Goodness, yakanunulika mitaani na ndani ya saa kumi tu, hakukuwa na gazeti lolote mitaani lililokuwa na habari kuhusu muigizaji huyo, yote yalikuwa yamenunuliwa.
Siku hiyo, watu wengi walijikusanya nje ya nyumba ya Goodness, kila mmoja alifika mahali hapo kwa lengo la kuwaona watoto hao na hata kutaka kumpa pole Goodness kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Alijua fika kwamba alikuwa akipendwa na watu hao walikuwa wamefika hapo kwa ajili ya kumuona yeye lakini hiyo haikumfanya kukubali kutoka nje kuonana na watu hao.
Tangazo lilipotolewa na PJ kwamba Goodness hakuwa tayari kutoka na kuonana nao, kila mmoja akalalamika, fujo zikaanza kutokea huku wengine wakipiga kelele na kutaka kumuona Goodness.
Japokuwa wasanii walijitahidi kwa nguvu zote kuwazuia watu hao, lakini hawakutulia, njia pekee ya kuwatuliza watu hao zaidi ya elfu tano ilikuwa ni kumruhusu Goodness kutoka ndani ya nyumba yake na kuonana nao tu.
“Imekuwaje?” aliuliza Mwenyekiti wa Bongo Muvi, Salim ambaye alikuwa akiitwa kwa jina la utani la Robert Mugabe.
“Watu wamekataa kuondoka, wanachotaka ni kumuona Goodness tu,” alisema Pj huku akionekana kukerwa na kelele zile.
“Daah! Sasa tufanye nini? Goodness amesema leo hawezi kuongea nao,” alisema Salim.
“Sijajua, jaribu kumshawishi atoke na aongee nao, la sivyo, hakukaliki hapa,” alishauri Pj.
Alichokifanya Salim ni kuelekea chumbani kwa Goodness. Wasanii wengi wa kike walikuwepo ndani ya chumba hicho huku kila mmoja akiwashika watoto wale. Salim akamwambia hali iliyokuwa ikiendelea nje, watu walikuwa wamegoma kuondoka mpaka atoke na kuongea nao.
“Nifanye nini? Nitoke au nisitoke?” Goodness alimuuliza Kei ambaye mbali na urafiki wao, alikuwa mshauri wake mkuu.
“Nenda kaongee nao, ila usitoke na watoto,” alishauri Kei.“Hakuna tatizo,” alisema Goodness na kuanza kujiandaa.Bado fujo ziliendelea nje ya nyumba ile, watu hao walikuwa wakitaka kumuona Goodness tu. Walipoona kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyetoka nje, wakaanza kuliimba jina la Goodness.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kilikuwa kikishangaza, Goodness alionekana kupendwa zaidi ya wasanii wengine. Filamu zake alizokuwa ameigiza, ziliwafanya watu kumpenda kwa mapenzi ya dhati.
“Tunataka kumuona yeye tu, tunajua kwamba watoto tutawaona, tunataka kumuona Goodness wetu,” alisema msichana mmoja aliyekuwa akihojiwa na waandishi wa habari waliokuwa wamekusanyika mahali hapo kwa ajili ya kupiga picha na kuchukua matukio yaliyokuwa yakiendelea.
Baada ya dakika kadhaa, Goodness akatoka nje. Watu wakapaza sauti zao za shangwe, hawakuamini kama mtu waliyekuwa wakimpenda, Goodness alikuwa amesikia vilio vyao na kutoka nje ya nyumba hiyo.
Mwili wake ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa, mawazo juu ya watoto wake yalimtesa kwa kipindi kirefu mno. Japokuwa alikuwa katika hali hiyo, watu hawakujali, walichokuwa wakitaka ni kumuona muigizaji huyo tu.
Watu hawakutulia, kumuona tu hakukutosha, wakataka kumsogelea na kumgusa. Hapo, fujo zikaanza upya, umati wa watu elfu tano, wote hao walikuwa wakitaka kumgusa Goodness tu jambo lililowafanya kuonekana kama watu waliokuwa kwenye maandamano ya kisiasa.
“PJ, wazuie,” alisema Kei.
“Nitawezaje kuwazuia watu elfu tano? Kama vipi aingie ndani,” alisema PJ.
“Hapana, kwa sababu wananipenda, acha tu waniguse,” alisema Goodness.
Mapenzi waliyoyaonesha watu hao yalikuwa makubwa, hakutaka kuwaacha hivihivi tu, kile walichokuwa wakikihitaji, basi alitaka kuwatimizia. Wakaambiwa wapange mstari kwani ndiyo ingekuwa njia rahisi ambayo ingewarahisishia, hilo halikuwa tatizo, wakajipanga.
Siku hiyo, ndani ya saa mbili, Goodness alikuwa na kazi moja tu, kusalimiana na watu hao kwa kuwashika mikono, alipomaliza, akaahidi kwamba yangefanyika mahojiano maalumu kuhusu kila kitu kilichotokea katika maisha yake alipokuwa nchini India.
“Nitaongea kupitia Global TV, nitaongea mengi,wala msiwe na wasiwasi,” alisema Goodness.
Waandishi wa televisheni hiyo walivyosikia hivyo, wakajipanga vilivyo, siku hiyo ilipofika, watu wakajikusanya mbele ya televisheni zao, kila mmoja alikuwa akitaka kusikia kilichokuwa kimeendelea nchini India.
Mamilioni ya watanzania, wakajiweka tayari, kitu walichokuwa wakikitaka ni kujua kipi kiliendelea nchini India na kwa nini watoto hawakutenganishwa, hicho ndicho hasa kilichokuwa kikitakiwa kujulikana mahali hapo.


EmoticonEmoticon